HABARI TANZANIA |TheOrigin of News.
Tanzania Social news| Politics|Sports & Entertainment.
Thursday, 18 August 2016
RAIS MAGUFULI ATENGUA UTEUZI WA MKUU WA MKOA WA ARUSHA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefanya mabadiliko madogo ya uongozi na kumteua Bw. Mrisho Gambo kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuanzia leo (Alhamisi, Agosti 18,2016).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Bw. Gambo anachukua nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Felix Kijiko Ntibenda ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Amesema Bw. Ntibenda anahamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa majukumu mengine.
Kabla ya uteuzi huo, Bw. Gambo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha. Ataapishwa kesho (Ijumaa, Agosti 19, 2016) saa 3 asubuhi Ikulu jijini Dar es Salaam.
IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU, 2 MTAA WA MAGOGONI, S. L. P. 3021, 11410 DAR ES SALAAM.
Wednesday, 17 August 2016
VYUO VILIVYOPOKEA FEDHA ZA WANAFUNZI HEWA VYAPEWA SIKU 7 KUZIRUDISHA.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ametoa siku saba kuanzia Agosti 17, 2016 kwa vyuo vikuu kurejesha fedha zilizopokea ambazo ni za wanafunzi ambao hawapo chuoni.
Prof. Ndalichako ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongea na waandishi wa habari juu ya taarifa la zoezi la uhakiki wa wanafunzi wanufaika wa mikopo vyuo vya Elimu juu.
Prof. Ndalichako amesema kuwa uhakiki wa wanafunzi hao umefanyika katika vyuo 31 kati ya vyuo 81 vilivyopo nchini, Katika utafiti huo wanafunzi 2,192 wameshindwa kuhakiki majina yao, hivyo kushindwa kuthibitisha uwepo na uhalali wa wanafunzi hao.
“Mikopo ya Wanafunzi hao imesitishwa na kwa wale ambao ni wanafunzi halali lakini walishindwa kujihakiki itabidi waombe tena mkopo,” alifafanua Mhe. Ndalichako.
Ameendelea kwa kusema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2015/16 wanafunzi hao hewa wameigharimu Serikali kiasi cha shilingi 3,857,754,460, kiasi ambacho kinatakiwa kurejeshwa na vyuo ambavyo wanafunzi hao wamebainika.
Aidha, Prof. Ndalichako amesema kuwa taarifa hiyo imekabidhiwa kwenye vyombo vya sheria ili kuwachukulia hatua wale wote watakaobainika kufanya udanganyifu na kusababisha Serikali hasara ya mabilioni ya fedha.
Vile vile Prof. Ndalichako amewataka wakuu wa vyuo kuweka mfumo wa kuhakiki usahihi wa matokeo ya wanafunzi yanayotumwa Bodi ya Mikopo kutokana na vyuo vingi kubainika kuwepo kwa udanganyifu mkubwa kwenye matokeo ya wanafunzi ambao hawakufanya mtihani au waliofeli na kuandikiwa wamefaulu ili waendelee kupata mikopo.
Tuesday, 16 August 2016
BAADA YA MANJI KUJIUZULU, HAYA NDIO MAAMUZI YA MKUTANO WA VIONGOZI WA YANGA
Viongozi wa klabu ya Yanga leo saa nne walikutana katika kikao cha dharura kufuatia mwenyekiti wa klabu hiyo, Yusuf Manji kutangaza kujiuzulu na kutupilia mbali mpango wake wa kutaka kuikodisha timu hiyo na kuiendesha kibiashara kwa miaka 10.
Manji alijiuzulu kwa tuhuma kuwa kuna baaadhi ya viongozi wa Yanga wamemkashafu na mmoja aliyetuhumiwa kwa kosa hilo ni Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee, Yahya Akilimali.
Maazimio ya Viongozi wa Matawi wa Yanga waliokutana leo katika kikao cha dharura Makao Makuu ya Yanga.
1. Viongozi hao wamelaani taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Wazee, Mzee Akilimali na kuwa haikuwa taarifa iliyopewa baraka na Yanga.
2. Viongozi wa Matawi wamemtaka Katibu Mkuu wa Yanga kumfuta uanachama wa Yanga Yahya Akilimali kwa kosa la kumkashifu mwenyekiti wa Yanga.
3. Katiba ya Yanga hailitambui Baraza la Wazee badala yake inalitambua Baraza la Wadhamini, hivyo basi viongozi wa Yanga wamemuomba Katibu Mkuu wa Yanga kuvunja Baraza la Wazee na wazee hao warudishwe katika matawi wawe wanachama wa kawaida.
4. Mwanachama yeyote wa Yanga atakayeongea na vyombo vya habari bila idhini ya Yanga, atakuwa amejifuta uanachama wake.
Kwa upande wa Mzee Yahya Akilimali alikuwa na haya ya kusema;-
Sijamtusi mwenyekiti wangu kwa kusema amekurupuka. Neno hilo ni la kawaida wala sikuwa na dhamira ya kumtusi mwenyekiti wangu, nawaomba radhi wana-Yanga kwa kauli zangu. Usiku sijalala nilikosa raha mara baada ya kusikia Manji kajiuzulu.
Mie naomba tuwe na umoja tatizo letu na mwenyekiti ni kushindwa kutuita wazee kwenye mpango wake wa kuichukua timu.
Sisi tunampenda na kumuhitaji sana Yusuf lakini tunahitaji aendeleze mfumo wa zamani alioanza nao wa kujali na kuthamini wazee ili nasi tujisikie vizuri na klabu yetu.
Nasisitiza sina chuki na Manji maana kwa mdomo wangu huu nimeshiriki sana kumuweka madarakani mpaka pale umma wa watanzania wakasema tumevunja katiba. Ninachotaka alitambue Baraza la Wazee na sisi tukae nae tuzungumze mstakabali wa klabu yetu.
Friday, 12 August 2016
SERIKALI YAZIKINGIA KIFUA SHULE ZA FEDHA ZA DAR.
SERIKALI imesema haina ushahidi wa kutosha kuzitia hatiani shule za Feza nchini zinazodaiwa kumilikiwa na mmoja wa wananchi wa Uturuki anayetuhumiwa kujihusisha na ugaidi na kuitaka Serikali ya Uturuki kuwasilisha taarifa zenye ushahidi wa kutosha kuhusu tuhuma hizo.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga.
Alisema walipokea madai kutoka Ubalozi wa Uturuki nchini kuwa shule hizo zinamilikiwa na mmoja wa wananchi wa nchi hiyo anayejihusisha na ugaidi.
Balozi Mahiga alisema katika madai ya ubalozi huo, shule hizo ni miongoni mwa miradi inayomilikiwa na mtuhumiwa huyo na kwamba, baadhi ya walimu wake hutumia mbinu za kigaidi kufundisha wanafunzi.
Akijibu tuhuma hizo, Balozi Mahiga alisema serikali kabla ya kutoa kibali kwa mwekezaji au mfanyabiashara yeyote kuendesha shughuli zake nchini, vyombo vya usalama nchini, hufanya upelelezi wa kina na wamejiridhisha kwamba wafanyabiashara wa Uturuki waliopo nchini wanafanya biashara halali.
“Ni kweli tumepokea tuhuma kutoka kwa Ubalozi wa Uturuki nchini kuhusu shule za Feza kwamba ni sehemu ya makundi ya kigaidi, lakini hatuwezi kuzitia hatiani shule hizo hadi tuletewe ushahidi wa kutosha,” alisema Balozi Mahiga.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule za Feza, Habib Miradji alisema shule hizo ni za asasi iliyosajiliwa kisheria na Serikali ya Tanzania hivyo ni mali ya Tanzania na endapo kuna kitu au tatizo ni lazima wawasiliane na serikali na watafika kukagua ili kama kuna lolote baya hatua zichukuliwe.
Aidha alisema kwamba shule hazijafungwa.
Thursday, 11 August 2016
GAZAETI LA MSETO LAPIGWA KUFULI KWA MIAKA 3
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeamua kulifungia kwa miezi 36 gazeti la “MSETO”. Amri ya kulifungia Gazeti hilo imetolewa kwa Tangazo la Serikali Na. 242 lililotolewa tarehe 10 Agosti, 2016. Uamuzi huo umetolewa kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya Mwaka 1976 Sura ya 229, kifungu 25(1).
Kifungu hicho kinasema “Waziri akiona kwamba kwa ajili ya manufaa ya umma au kwa ajili ya kudumisha amani na usalama inafaa afanye hivyo aweza kutoa amri na kuitangaza kwenye Gazeti la Serikali ambayo itaeleza kwamba gazeti lililotajwa katika amri hiyo litakoma kutolewa tangu siku (ambayo katika fungu hili itaitwa ''tarehe ya kuanza kutumika'') itakayotajwa katika amri hiyo”
Uamuzi huo unazuia gazeti la Mseto kuchapishwa katika njia nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na mitandao (Online publication) kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Sura ya 306.
Aidha, hatua hii ya kulifungia gazeti hilo imechukuliwa baada ya Msajili wa Magazeti kufanya juhudi kubwa za muda mrefu kuanzia Septemba, 2012 hadi Agosti, 2016 kumtaka Mhariri wa gazeti kuacha kuandika habari za upotoshaji, uchochezi na za uongo na zisizo zingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari bila mafanikio.
Kutokana na hali hiyo, Serikali kwa masikitiko makubwa, imelazimika kuchukua uamuzi huu kutokana na mwenendo wa uandishi wa gazeti hilo wa kuandika na kuchapisha habari ya uongo na kughushi kwa kutumia nyaraka mbalimbali za Serikali kwa nia ya kumchafua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na viongozi wa Serikali kwa lengo kutaka kumchonganisha na wananchi ambao wamekuwa na matarajio makubwa kwa uongozi wa Awamu ya Tano.
Pamoja na makosa mengine, hivi karibuni gazeti lao katika toleo Na. 480 la tarehe 4 hadi 10 Agosti, 2016 lilichapisha na kusambaza makala na barua ya kugushi kutoka Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) yenye kichwa cha habari kisemacho “Waziri Amchafua JPM” Amhusisha na rushwa ya uchaguzi mkuu, ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano.
Kwa mujibu wa vyombo vya uchunguzi vya Serikali, imebainika kwamba nyaraka hiyo imeghushiwa na wahariri na walipotakiwa kuleta uthibitisho wa nyaraka waliyotumia katika gazeti lao, walishindwa kuleta vithibitisho hivyo
Ninatoa wito kwa wamiliki, wahariri, waandishi na watangazaji wa habari kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ambayo ukizingatiwa hakutakuwa na migogoro yoyote. Aidha Serikali inasisitiza kwamba inaheshimu uhuru wa vyombo vya habari unaozingatia maadili, weledi na Sheria za nchi na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana navyo.
Serikali ya Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayoanisha uhuru na mipaka ya habari kama vile Tamko la Kimataifa la haki za Binadamu la mwaka 1948, Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa, na Mkataba wa Afrika juu ya Haki za Binadamu na Watu 1981.
Mikataba na matamko hayo kwa pamoja licha ya kuanisha uhuru wa habari ambao Tanzania imeruhusu kwa kiwango kikubwa pia, imeweka ukomo wa uhuru huo kwa kukataza habari za uongo, uzushi na uchochezi.
Ninapenda kusisitiza kwamba Serikali itaendelea kujenga uhusiano mzuri na wa kirafiki kati yake na wadau wa sekta ya habari. Aidha ninasisitiza tena wadau wa sekta hii kuzingatia Sheria, kanuni na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari ili kujenga heshima ya tasnia ya habari na kulinda amani ya nchi yetu.
Mhe. Nape M. Nnauye (Mb,) WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI,SANAA NA MICHEZO.
Tuesday, 9 August 2016
POLISI KUFUTA VYUO VYA VETA VISIVYO NA SIFA
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema litavifungia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya udereva nchini bila ya kuwa na sifa.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishina wa Polisi (DCP) Mohamed Mpinga wakati akifungua mkutano wa pili wa Chama cha Shule Binafsi za Udereva Tanzania (Chashubuta) uliofanyika Dar es Salaam jana.
"Kuanzia sasa Jeshi la Polisi halitasita kukifungia chuo chochote cha udereva kitakachokosa sifa kwani kwa kulea shule mbovu tutaendelea kupata ajali na hivyo kuongeza vifo na majeruhi" alisema Mpinga.
Mpinga alisema kwa mujibu wa sheria ya shule za udereva sura 163 ya 1965 (R.E 2002) mpaka sasa jeshi la polisi limesajili shule za udereva 260 ambazo zitategemewa kutoa madereva bora wenye ueledi wa kutosha kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha ajali ni makosa ya kibinadamu ambayo yanafanywa na madereva.
Alisema jeshi hilo litafanya msako nchi nzima kuvibaini vyuo ambavyo havina sifa na wamiliki wake kuchukuliwa hatua na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.
Mwenyekiti wa Chashubuta Taifa, Robert Mkolla wakati akisoma risala yao mbele ya Mpinga ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mkutano huo, alisema moja ya changamoto waliyonayo ni baadhi ya wadau wa sekta ya usafiri na usafirishaji kutoona mchango mkubwa unaofanywa na shule za udereva za watu binafsi wakiamini kuwa vyuo vinavyotoa elimu nzuri ni vile vya serikali pekee.
Mkolla alimuomba Kamanda Mpinga uboreshwaji wa mitaala mara kwa mara ili kwenda na mahitaji ya barabara, vyombo na wakati na shule hizo ziwe zinashirikishwa katika kutoa michango ya uboreshaji mitaala hiyo
POLISI KUFUTA VYUO VYA VETA VISIVYO NA SIFA
JESHI la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limesema litavifungia vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya udereva nchini bila ya kuwa na sifa.
Kauli hiyo ameitoa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Kamishina wa Polisi (DCP) Mohamed Mpinga wakati akifungua mkutano wa pili wa Chama cha Shule Binafsi za Udereva Tanzania (Chashubuta) uliofanyika Dar es Salaam jana.
"Kuanzia sasa Jeshi la Polisi halitasita kukifungia chuo chochote cha udereva kitakachokosa sifa kwani kwa kulea shule mbovu tutaendelea kupata ajali na hivyo kuongeza vifo na majeruhi" alisema Mpinga.
Mpinga alisema kwa mujibu wa sheria ya shule za udereva sura 163 ya 1965 (R.E 2002) mpaka sasa jeshi la polisi limesajili shule za udereva 260 ambazo zitategemewa kutoa madereva bora wenye ueledi wa kutosha kutokana na kuwa chanzo kikubwa cha ajali ni makosa ya kibinadamu ambayo yanafanywa na madereva.
Alisema jeshi hilo litafanya msako nchi nzima kuvibaini vyuo ambavyo havina sifa na wamiliki wake kuchukuliwa hatua na kuwafikisha kwenye mkono wa sheria.
Mwenyekiti wa Chashubuta Taifa, Robert Mkolla wakati akisoma risala yao mbele ya Mpinga ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mkutano huo, alisema moja ya changamoto waliyonayo ni baadhi ya wadau wa sekta ya usafiri na usafirishaji kutoona mchango mkubwa unaofanywa na shule za udereva za watu binafsi wakiamini kuwa vyuo vinavyotoa elimu nzuri ni vile vya serikali pekee.
Mkolla alimuomba Kamanda Mpinga uboreshwaji wa mitaala mara kwa mara ili kwenda na mahitaji ya barabara, vyombo na wakati na shule hizo ziwe zinashirikishwa katika kutoa michango ya uboreshaji mitaala hiyo
Subscribe to:
Comments (Atom)